Ruka hadi Yaliyomo
AfroCave

Kifungu 75. Mienendo ya Maafisa wa Serikali

(1) Afisa wa Serikali atakuwa na mienendo iliyonyooka, iwe katika maisha yake ya kuhudumia umma na afisi, katika maisha ya kibinafsi, au katika kuingiliana na watu wengine, yeye atapaswa kudumisha mienendo itakayomwepusha na–

  • (a) mgongano wowote kati ya maslahi ya kibinafsi na wajibu wake wa kuhudumia umma au afisi;
  • (b) ukiukaji wa maslahi yoyote ya umma au kiafisi kwa ajili ya maslahi yake ya kibinafsi; au
  • (c) kudhalilisha afisi au cheo anachoshikilia afisa huyo.

(2) Afisa wa Serikali anayetenda kinyume na ibara ya (1), au Kifungu cha 76, 77 au 78 (2)–

  • (a) atawekwa chini ya taratibu za kinidhamu zinazotumika kwa afisi inayohusika;
  • (b) kulingana na taratibu za kinidhamu zilizotajwa katika aya ya (a), anaweza kuachishwa kazi au vinginevyo, kuondolewa afisini.

(3) Mtu ambaye ameachishwa kazi au vinginevyo kutolewa afisini kwa kukiuka vipengele vilivyotajwa katika ibara ya (2) atapigwa marufuku kushikilia afisi yoyote nyingine ya Serikali.