Ruka hadi Yaliyomo
AfroCave

Kifungu 73. Majukumu ya Uongozi

(1) Mamlaka yaliyotolewa kwa afisa wa Serikali–

  • (a) ni amana ya umma inayopaswa kutekelezwa katika njia ambayo–
    • (i) inaambatana na majukumu na makusudi ya Katiba hii;
    • (ii) inadhihirisha heshima kwa watu;
    • (iii) inaleta sifa katika taifa na hadhi kwenye afisi; na
    • (iv) inakuza imani ya umma katika maadili ya kiafisi; na
  • (b) yanampa afisa huyo wa Serikali jukumu la kuhudumia watu badala ya nguvu za kuwatawala.

(2) Kanuni zinazotoa mwongozo wa uongozi na maadili ni–

  • (a) uteuzi kwa misingi ya uadilifu, ustadi wa kufanya kazi, kufaa kwake, au uchaguzi huru na wa haki;
  • (b) kutopendelea katika maamuzi na katika kuhakikisha kwamba maamuzi hayo hayatokani na mapendeleo ya kindugu au nia zingine zozote mbaya au vitendo vya ufisadi;
  • (c) huduma za kujitolea kwa misingi hasa ya manufaa ya umma, ikidhihirishwa na–
    • (i) uaminifu katika utekelezaji wa wajibu kwa umma; na;
    • (ii) kutangaza maslahi ya kibinafsi yanayoweza kugongana na wajibu wake kwa umma;
  • (d) uwajibikaji kwa umma kuhusu maamuzi na hatua zinazochukuliwa; na
  • (e) nidhamu na kujitolea katika kuhudumia watu.