Ruka hadi Yaliyomo
AfroCave

Kifungu 232. Maadili na Kanuni za Huduma za Umma

(1) Maadili na Kanuni za Umma huhusisha–

 • (a) viwango vya juu vya maadili ya kitaaluma;
 • (b) matumizi bora ya rasilmali;
 • (c) utoaji wa haraka wa huduma za umma usio na upendeleo na unaozingatia usawa na haki;
 • (d) ushirikishwaji wa watu katika utaratibu wa kuunda Sera;
 • (e) uwajibikaji katika shughuli za kiusimamizi;
 • (f) uwazi na utoaji wa habari sahihi kwa umma bila kuchelewa;
 • (g) kwa kuzingatia ibara za (h) na (i), ustahili na ujuzi wa mtu ndio msingi wa kuteuliwa au kupandishwa cheo;
 • (h) uwakilishi wa jamii mbalimbali za Kenya; na
 • (i) kutoa nafasi sawa na za kutosha za kazi, katika kuteua, kutoa mafunzo na kupandishwa vyeo katika ngazi zote zahuduma za umma, kwa–
  • (i) wanaume na wanawake;
  • (ii) watu wa jamii zote; na
  • (iii) watu wenye ulemavu.

(2) Maadili na Kanuni za Huduma za umma huhusisha huduma za umma kwa–

 • (a) idara zote za serikali katika viwango vyote viwili vya serikali; na
 • (b) mashirika yote ya serikali.

(3) Bunge litaunda sheria kukipa nguvu Kifungu hiki.