Ruka hadi Yaliyomo
AfroCave

Kifungu 229. Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu

(1) Kutakuwa na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu atakayependekezwa na Rais, kuidhinishwa na Baraza la Kitaifa na kuteuliwa na Rais.

(2) Kuhitimu kuwa Mkaguzi, mtu lazima awe na ujuzi mkubwa wa masuala ya fedha za umma au tajriba isiyopungua miaka kumi katika ukaguzi wa usimamizi wa fedha za umma.

(3) Msimamizi huyu atakuwa afisini kwa mujibu wa Kifungu cha 251, kwa kipindi cha miaka nane na hawezi tena kuteuliwa upya.

(4) Kati ya miezi sita baada ya kukamilika kwa kila mwaka wa fedha, Mkaguzi Mkuu atakagua na kutoa ripoti, kwa mujibu wa mwaka huo wa fedha, kuhusu–

  • (a) hesabu za serikali ya taifa na serikali za kaunti;
  • (b) hesabu za hazina zote na mashirika ya serikali ya kitaifa na ya serikali za kaunti;
  • (c) hesabu za mahakama zote;
  • (d) hesabu za kila Tume na Afisi huru zote zilizoundwa na Katiba hii;
  • (e) hesabu za Baraza la Kitaifa, Seneti na mabaraza ya kaunti;
  • (f) hesabu za fedha za vyama vya kisiasa zinazotoka kwenye hazina za umma;
  • (g) deni la umma; na
  • (h) hesabu za shirika lingine lolote ambalo linatakiwa kisheria kufanyiwa ukaguzi na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu.

(5) Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu anaweza kukagua na kutoa ripoti za hesabu za shirika lolote linalopokea fedha kutoka hazina za umma.

(6) Ripoti ya ukaguzi itathibitisha iwapo fedha za umma zimetumiwa kwa mujibu wa sheria au zilivyonuiwa.

(7) Ripoti za ukaguzi zitawasilishwa bungeni au kwenye mabaraza husika ya kaunti.

(8) Kati ya miezi mitatu baada ya kupokea ripoti ya ukaguzi, bunge au baraza la kaunti litazingatia na kujadili ripoti hizi na kuchukua hatua zifaazo.