Ruka hadi Yaliyomo
AfroCave

Kifungu 115. Idhini ya Rais na Urejeshaji

(1) Katika kipindi cha muda wa siku kumi na nne baada ya kupokea Mswada, Rais–

  • (a) ataweka saini; au
  • (b) ataurejesha Mswada Bungeni ili kuchunguzwa upya na Bunge huku likitilia maanani sababu alizo nazo Rais za kutouidhinisha mswada huo.

(2) Iwapo Rais ataurejesha Mswada bungeni kuchunguzwa upya, Bunge kwa kuzingatia taratibu zinazofaa kama zilivyotajwa katika sehemu hii, linaweza–

  • (a) kuurekebisha Mswada huo kwa kuangazia sababu muhimu alizotoa Rais; au
  • (b) kuupitisha Mswada huo kwa mara ya pili bila kufanya marekebisho.

(3) Iwapo Bunge limerekebisha Mswada huo huku likitilia maanani kikamilifu hoja za Rais, Spika anayehusika atampelekea Rais tena ili aweke sahihi.

(4) Bunge, baada ya kutilia maanani sababu za Rais,linaweza kuupitisha Mswada huo kwa mara ya pili bila marekebisho au ukiwa na marekebisho ambayo hayakuyapa nafasi kwa kikamilifu hoja za Rais kwa kura ambayo itaungwa mkono na–

  • (a) Thuluthi mbili ya wabunge wa Baraza la Kitaifa; na
  • (b) Thuluthi mbili ya uwakilishi katika Seneti, iwapo ni Mswada unaohitaji idhini ya Seneti.

(5) Iwapo Bunge litapitisha Mswada chini ya ibara ya (4)–

  • (a) Spika wa Bunge husika atahitajika baada ya siku saba auwakilishe tena mswada huo kwa Rais; na
  • (b) Rais atauwekea sahihi Mswada huo katika muda wa siku saba.

(6) Iwapo Rais hatauwekea sahihi Mswada huo au kuurejesha kwa wakati unaopendekezwa katika Ibara ya (1), au au aweke sahihi chini ya ibara ya (5) (b), mswada huo utachukuliwa kama ulioidhinishwa kufikia kumalizika kwa kipindi hicho.