Ruka hadi Yaliyomo
AfroCave

Kifungu 110. Miswada Kuhusu Serikali za Kaunti

(1) Katika Katiba hii, “Mswada unaohusu serikali ya kaunti” unamaanisha–

  • (a) mswada ulio na masharti yanayoathiri majukumu na mamlaka ya serikali za kaunti zilizotajwa katika Mpangilio wa Nne;
  • (b) Mswada unaohusiana na uchaguzi wa mwanachama wa bunge la kaunti au serikali za kaunti; na
  • (c ) mswada uliotajwa katika Sura ya Kumi na mbili unaoathiri fedha za serikali za kaunti.

(2) Mswada unaohusu serikali za kaunti ni–

  • (a) mswada maalumu ambao utashughulikiwa chini ya Kifungu cha 111, iwapo–
    • (i) unahusiana na uchaguzi wa wabunge wa bunge la kaunti au serikali ya kaunti; au
    • (ii) ni Mswada wa Mgao wa Mapato ya Kaunti wa kila mwaka uliotajwa katika Kifungu cha 218; au
  • (b) mswada wa kawaida ambao utashughulikiwa chini ya Kifungu cha 112 katika hali yoyote.

(3) Kabla ya mojawapo ya vitengo vya Bunge kutathmini mswada, Maspika wa Baraza la Kitaifa na Seneti kwa pamoja wataamua suala lolote kuhusu kama Mswada huo unahusu kaunti na iwapo ni hivyo, kama ni mswada maalumu au wa kawaida.

(4) Wakati Mswada unahusu serikali za kaunti umepitishwa na Bunge moja, Spika wa Bunge hilo ataupeleka kwa Spika wa Bunge hilo jingine.

(5) Iwapo Mabunge yote mawili yatapitisha Mswada katika mfumo uleule, Spika wa Bunge ulikotoka mswada huo, ataupeleka kwa Rais katika muda wa siku saba ili uidhinishwe.