Ruka hadi Yaliyomo
AfroCave

Kifungu 11. Utamaduni

(1) Katiba hii inatambua utamaduni kama msingi wa taifa na jumla ya ustaarabu wa watu na taifa la Kenya.

(2) Serikali–-

  • (a) itakuza aina zote za kitaifa na kitamaduni za kujieleza kupitia fasihi, sanaa, sherehe za kitamaduni, sayansi, mawasiliano, habari, vyombo vya habari, uchapishaji, maktaba na turathi nyingine za kitamaduni;
  • (b) itatambua jukumu la sayansi na teknolojia za kiasili katika maendeleo ya nchi;
  • (c) itatambua haki za kiubunifu za watu wa Kenya;

(3) Bunge litatunga sheria–

  • (a) kuhakikisha kwamba jamii zinapewa fidia au mrabaha kwa kutumiwa kwa turathi zao za kitamaduni; na
  • (b) kutambua na kulinda umiliki wa mbegu na mimea mbalimbali ya kiasili, sifa tofauti za kimaumbile na matumizi yake miongoni mwa jamii za Kenya.