Ruka hadi Yaliyomo
AfroCave

Kifungu 217. Mgao Unaolingana wa Mapato

(1) Mara moja baada ya kila miaka mitano, Baraza la Seneti litatoa mapendekezo kuhusu misingi ya kutumiwa katika ugavi wa mapato ya kitaifa yanayogawiwa kila serikali ya kaunti kila mwaka.

(2) Katika kutoa mapendekezo ya vigezo vya kutumiwa kugawa mapato yaliyotajwa katika ibara ya (1), Seneti–

 • (a) itatilia maanani kigezo katika kifungu cha 203 (1);
 • (b) itaitisha na kuzingatia mapendekezo ya Tume ya Ugavi wa Mapato;
 • (c) itawashauri Magavana wa serikali za kaunti, Waziri anayesimamia fedha na asasi nyingine yoyote ya serikali ya kaunti; na
 • (d) itawaalika watu, ikiwa ni pamoja na makundi ya wataalamu, kutoa mapendekezo yao.

(3) Katika kipindi cha kati ya siku kumi baada ya Seneti kuidhinisha pendekezo chini ya ibara ya (1), Spika wa Seneti atawasilisha pendekezo hilo kwa Spika wa Baraza la Kitaifa.

(4) Katika kipindi cha kati ya siku sitini baada ya maamuzi ya Seneti kuwasilishwa kama inavyotajwa katika ibara ya (3), Baraza la Kitaifa litachunguza pendekezo hilo na kulipigia kura ili kuliidhinisha kwa kulifanyia au kutolifanyia marekebisho, au kulikataa.

(5) Ikiwa Baraza la Kitaifa–

 • (a) halitapiga kura kwa pendekezo hili kwa kipindi cha siku sitini, basi itachukuliwa kwamba pendekezo hili limeidhinishwa na Baraza la Kitaifa bila marekebisho;
 • (b) litapiga kura kwa pendekezo hili, pendekezo litakuwa–
  • (i) limefanyiwa marekebisho iwapo wajumbe wasiopungua thuluthi mbili wataunga mkono marekebisho;
  • (ii) litakatiliwa iwapo tu wajumbe wa bunge wasiopungua thuluthi mbili watalipigia kura ya kulikataa, bila kujali kama limefanyiwa marekebisho na Baraza la Kitaifa au la; au
  • (iii) kuidhinishwa, kwa njia yoyote ile.

(6) Iwapo Baraza la Kitaifa litaidhinisha pendekezo lililofanyiwa marekebisho au kulikataa pendekezo, basi Seneti itakuwa na uchaguzi wa–

 • (a) kuchukua pendekezo jipya chini ya ibara ya (1), katika hali hii masharti ya ibara ya (4) na (5) yatatumiwa upya;
 • (b) kuomba suala hili liwasilishwe kwa kamati ya pamoja ya mabaraza yote mawili ya Bunge kwa upatanisho chini ya kifungu cha 113, utakaozingatia marekebisho muhimu.

(7) Pendekezo hili chini ya kifungu hiki kitakachokuwa kimeidhinishwa chini ya ibara ya (5) basi kitaendelea kutekelezwa hadi wakati ambapo pendekezo jipya litakapoidhinishwa.

(8) Licha ya ibara ya (1), Seneti, kwa uamuzi ikiwa umeungwa mkono na wanachama wasiopungua thuluthi mbili, inaweza kulifanyia marekebisho pendekezo lililoidhinishwa.

(9) ibara ya (2) hadi (8), na marekebisho muhimu, zinataja pendekezo chini ya ibara ya (8).