Ruka hadi Yaliyomo
AfroCave

15. Masharti ya Ugatuzi wa Majukumu Kuidhinishwa na Sheria ya Bunge

(1) Kwa kuweka sheria, Bunge litatoa mwongozo wa kuhamisha kwa awamu, kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitatu, tokea wakati wa uchaguzi wa kwanza wa mabaraza ya kaunti, tokea serikali ya kitaifa hadi serikali za kaunti, majukumu yaliyopewa serikali hizo chini ya Kifungu cha 185.

(2) Sheria inayotajwa katika ibara ndogo ya (1)–

  • (a) kutoa mwongozo wa jinsi serikali ya kitaifa–
    • (i) itakavyosaidia katika ugatuzi wa mamlaka;
    • (ii) itakavyosaidia serikali za kaunti kujenga uwezo wao wa kujitawala na kutoa huduma zinazostahili kutoa; na
    • (iii) itakavyozisaidia serikali za kaunti;
  • (b) kuweka masharti yatakoyotimizwa kabla ya majukumu fulani kugatuliwa kwenda kwa serikali za kaunti, ili kuhakikisha kuwa serikali hizo hazipewi majukumu ambayo haziwezi kuyatekeleza; na
  • (c) kuruhusu ugatuzi wa mamlaka ili kuhakikisha kwamba majukumu yanagatuliwa kwa haraka kwa kaunti zile ambazo zina uwezo wa kuyatekeleza na kwamba pasiwe na kaunti ambayo imepewa majukumu isiyoweza kutekeleza; na
  • (d) kutoa utaratibu utakaohakikisha kwamba Tume ya Utekelezaji wa Katiba itatekeleza wajibu wake wa kufuatilia utekelezaji wa mfumo wa ugatuzi sawasawa.