Ruka hadi Yaliyomo

Kifungu 89. Kuwekea Mipaka Maeneo ya Uchaguzi

(1) Kutakuwa na maeneobunge mia mbili tisini kwa lengo la uchaguzi wa wabunge wa Baraza la Kitaifa kama ilivyotajwa katika Kifungu cha 97 (1) (a).

(2) Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka itarekebisha upya majina na mipaka ya maeneobunge kila baada ya muda usiopungua miaka minane na usiozidi miaka kumi na miwili, lakini marekebisho yoyote lazima yakamilishwe angalau miezi kumi na miwili kabla ya uchaguzi mkuu wa wabunge.

(3) Tume itarekebisha upya mara kwa mara idadi, majina na mipaka ya wadi.

(4) Ikiwa uchaguzi mkuu utafanyika katika kipindji cha miezi kumi na miwili baada ya kukamilika kwa marekebisho yatakayoendeshwa na Tume, mipaka hiyo mipya haitatekelezeka kwa ajili ya uchaguzi huo.

(5) Mipaka ya kila eneobunge italinganishwa kwa, inakaribiana sana, sawa na idadi ya wakazi katika eneobunge hilo, lakini idadi ya wakazi wa eneobunge inaweza kuwa kubwa au ndogo kuliko idadi ya kiasi cha watu kwa namna ambayo imetajwa katika Ibara ya (6) ili kuzingatia–

  • (a) hali ya kijiografia na maeneo ya miji;
  • (b) jamii ya eneo lile, kihistoria, kiuchumi na mshikamano wake wa kitamaduni; na
  • (c) mbinu za mawasiliano.

(6) Idadi ya wakazi wa eneobunge au wadi inaweza kuwa kubwa au ndogo zaidi ya idadi ya watu kwenye eneo hilo kwa kiwango kisichozidi–

  • (a) asilimia arubaini kwa majiji na maeneo yaliyo na idadi ya watu iliyotawanyika; na
  • (b) asilimia thelathini kwa sehemu nyingine.

(7) Katika kurekebisha mipaka ya maeneobunge na wadi, Tume–

  • (a) itashauriana na makundi yote husika; na
  • (b) itandelea kufanya kazi kwa lengo la kuhakikisha kwamba idadi ya watu katika kila eneobunge na wadi, inakaribiana, sawa na idadi ya watu wa eneo hilo iliyokadiriwa.

(8) Ikiwezekana, Tume hii itabadilisha majina na mipaka ya maeneobunge na wadi, na idadi, majina na mipaka ya wadi.

(9) Kulingana na Ibara ya (1) (2),(3) na (4), majina na maelezo ya kina kuhusu mipaka ya maeneobunge na wadi iliyobuniwa na Tume, itachapishwa kwenye Gazeti Rasmi la Serikali, na itatekelezwa baada ya kuvunjwa kwanza kwa Bunge, kufuatia kuchapishwa kwake.

(10) Mtu anaweza kutuma maombi kwa Mahakama Kuu ili kubatilisha maamuzi yaliyo chini ya kifungu hiki na yaliyotolewa na Tume.

(11) Ombi la kurekebisha maamuzi yaliyotolewa chini ya Kifungu hiki, litatumwa katika kipindi cha siku thelathini baada ya uchapishaji wa uamuzi uliopo kwenye Gazeti Rasmi la Serikali na litasikilizwa na kuamriwa katika kipindi cha miezi mitatu kutoka siku ya kuwasilishwa kwa ombi hilo.

(12) kwa sababu ya Kifungu hiki, ‘ idadi ya watu’ ina maana ya idadi inayopatikana baada ya kugawa idadi ya watu wanaoishi Kenya kwa idadi ya maeneobunge au wadi, ifaavyo, kwa namna ambayo, Kenya ilivyogawanywa chini ya Kifungu hiki.