Ruka hadi Yaliyomo
AfroCave

Kifungu 88. Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka

(1) Kutabuniwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka.

(2) Mtu hastahili kuteuliwa kama mwachama wa Tume, ikiwa mtu huyo–

 • (a) ashawahi kushikilia afisi au kugombea uchaguzi katika kipindi cha miaka mitano iliyotangulia kama–
  • (i) mbunge katika ama mbunge kwenye bunge la kaunti; au
  • (ii) mwanachama wa taasisi ya kiserikali inayosimamia chama cha kisiasa; au
 • (b) anashikilia afisi yoyote ya taifa.

(3) Mwanachama wa Tume hatashikilia afisi nyingine ya umma.

(4) Tume inawajibika kuendesha na kusimamia kura za maamuzi na chaguzi katika taasisi zote zinazofanya uchaguzi au afisi zilizobuniwa na Katiba hii, na chaguzi nyingine zozote kama zilivyoagizwa na kifungu cha Sheria ya Bunge na hususan, katika–

 • (a) usajili wa mara kwa mara wa raia kama wapiga kura;
 • (b) usahihishaji wa mara kwa mara kwa kitabu cha usajili ya wapiga kura;
 • (c) kuweka mipaka ya maeneobunge na wadi;
 • (d) kudhibiti taratibu ambazo vyama hutumia kuteua wagombea uchaguzi;
 • (e) kusuluhisha mizozo ya uchaguzi, ikiwa ni pamoja na mizozo inayohusiana na au kutokana na uteuzi lakini isiyohusisha malalamiko ya uchaguzi na mizozo inayotokana na kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi;
 • (f) kusajili wagombea uchaguzi;
 • (g) elimu ya mpigakura;
 • (h) kuwezesha uchunguzi, usimamizi na tathmini ya chaguzi;
 • (i) kudhibiti kiwango cha fedha zinazoweza kutumiwa na au kwa niaba ya mgombea au chama katika uchaguzi wowote;
 • (j) kujenga kanuni za uchaguzi kwa wagombea na vyama vinavyogombea uchaguzi katika uchaguzi; na
 • (k) kuchunguza utimizaji wa sheria inayotakikana chini ya Kifungu cha 82 (1) (b) kuhusiana na uteuzi wa wagombea wa vyama.

(5) Tume itatumia mamlaka yake kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Katiba hii na sheria ya kitaifa iliyotungwa bungeni.