Ruka hadi Yaliyomo
AfroCave

Kifungu 260. Ufasiri

Isipokuwa pale ambapo muktadha unahitaji vinginevyo, katika Katiba hii–

“mtu mzima” inamaanisha mtu ambaye amefikisha umri wa miaka kumi na minane;

“kitendo sawazishi” huhusisha hatua yoyote inayolenga kuondolea mbali ukosefu wa usawa au kumnyima mtu au kuingilia uhuru wake wa kimsingi;

“mtoto” inamaanisha mtu ambaye hajatimiza umri wa miaka kumi na minane;

“kukiuka” inahusisha kukosa kufanya inavyostahili;

“sheria ya kaunti” inamaanisha sheria iliyotungwa na serikali ya kaunti au chini ya mamlaka yaliyopewa baraza la kaunti;

“ulemavu” inahusisha ulemavu wowote wa kimwili, kihisia, kiakili, kisaikolojia au ulemavu wa aina nyingine, hali au ugonjwa ambao, au unaochukuliwa na sekta mahususi za kijamii kuwa na athari za muda mrefu kwa mtu kuweza kutekeleza majukumu yake ya kawaida ya kila siku;

“stakabadhi” inahusisha–

 • (a) chapisho lolote au suala lolote lililoandikwa, kuelezwa au kuandikwa juu ya kitu kwa kutumia herufi, michoro au alama au zaidi ya mojawapo ya njia hizo ambayo inadhamiriwa kutumiwa au inaweza kutumiwa kwa ajili ya kurekodi suala hilo; na
 • (b) majalada ya kielektroniki;

“tarehe ya kutekelezwa” inamaanisha tarehe ambayo Katiba hii ilianza kutumika;

“ kushindwa” inahusisha kukataa;

“mwaka wa fedha” inamaanisha kipindi cha miezi kumi na miwili kinachomalizika katika siku ya thelathini ya mwezi wa Juni au siku nyingine iliyoelezwa na sheria ya kitaifa, lakini mwaka wa mwanzo wa fedha wa asasi yoyote ni kipindi cha wakati tangu ilipoanza mpaka mara tu kufikia siku ya thelathini ya Juni, au siku yoyote ile itakayoelezwa na sheria ya kitaifa;

“Gazeti” inamaanisha Gazeti Rasmi la Serikali linalochapishwa kutokana na kibali cha serikali ya kitaifa, au gazeti jingine linalochapishwa pamoja na Gazeti rasmi la Kenya;

“dhamana” inamaanisha ahadi kamili au ahadi yenye masharti, kujitolea kwa serikali ya kitaifa kulipa nusu au kulipa kabisa mkopo wowote wa serikali ya kaunti au wa mtu yeyote;

“afisa wa mahakama” inamaanisha msajili, naibu wa msajili, hakimu, Kadhi au afisa msimamizi wa mahakama yaliyoundwa chini ya Kifungu cha 169 (1) (d);

“ardhi” inahusisha–

 • (a) eneo juu ya ardhi au chini ya mwamba;
 • (b) eneo lolote la maji au chini ya ardhi;
 • (c ) maji ya bahari katika eneo la bahari kwenye mipaka ya nchi na la kiuchumi;
 • (d) maliasili zilizopo juu au chini ya ardhi; na
 • (e) eneo la anga juu ya ardhi;

“utungaji sheria” unahusisha–

 • (a) Sheria ya Bunge, au sheria iliyotungwa chini ya mamlaka yaliyotolewa na sheria ya Bunge; au
 • (b) sheria iliyotungwa na baraza la serikali ya kaunti, au chini ya mamlaka yaliyotolewa na sheria kama hiyo;

“ mkopo” unajumlisha njia yoyote ya kukopa, kukopesha au malipo ya baadaye ambapo pesa kutoka kwa mfuko wa umma zinaweza kutumiwa, au zinahitaji kutumiwa ili kulipa au kulipia tena;

“jamii iliyotengwa” inamaanisha–

 • (a) jamii ambayo kutokana na idadi ndogo ya watu wake, au kwa sababu nyingineyo, imeshindwa kushiriki kikamilifu katika ujumla wa shughuli za maisha ya kijamii na kiuchumi ya Kenya;
 • (b) jamii ya kitamaduni, ambayo kutokana na hamu ya kuhifadhi utamaduni wake wa kipekee na utambulisho wake ili usimezwe, imebakia nje ya ujumla wa maisha ya kijamii na kiuchumi ya Kenya;
 • (c) jamii asilia ambayo imebakia kudumisha maisha na mitindo ya kitamaduni inayojikita kwenye uchumi wa shughuli za usasi na ukusanyaji; au
 • (d) wafugaji au jamii za ufugaji, ikiwa ni–
  • (i) wa kuhamahama; au
  • (ii) jamii zinazoishi mahala pamoja ambazo, kwa sababu ya kutengwa kijiografia, hazijashirikishwa kikamilifu katika shughuli za kijumla za kijamii na kiuchumi za Kenya.

“kundi lililotengwa” inamaanisha kundi la watu ambalo, kutokana na sheria au mazoea kabla, wakati wa, au baada ya tarehe ya utekelezaji wa Katiba hii, walikuwa wamebaguliwa katika mojawapo au zaidi ya misingi inayotajwa katika Kifungu cha 27 (4);

“sheria ya kitaifa” inamaanisha sheria ya Bunge, au sheria inayotungwa chini ya mamlaka ya Sheria ya Bunge;

“maliasili” inamaanisha vitu au hali za kimaumbile zisizo za kibinadamu ambazo zinaweza kutumiwa tena au zisitumiwe, pamoja na–

 • (a) mwanga wa jua;
 • (b) maji kwenye ardhi na chini ya ardhi;
 • (c) misitu, uanuwai wa kiasili na kinasaba, na
 • (d) miamba, madini, malighafi ya mafuta na vianzo vingine vya kawi.

“mzee katika jamii” inamaanisha mtu ambaye amefikisha umri wa miaka sitini;

“chama cha kisiasa” inamaanisha muungano wa watu uliobuniwa kwa madhumuni ambayo yametajwa katika sehemu ya 3 ya sura ya saba;

“mali” inahusisha nia au haki ya, au inayotokana na–

 • (a) ardhi au vitu vya kudumu kwenye ardhi, au kustawisha ardhi
 • (b) bidhaa au mali ya kibinafsi;
 • (c) hakimiliki au
 • (d) fedha au vifaa.

“afisa wa umma” inamaanisha–

 • (a) afisa yeyote wa serikali; au
 • (b) mtu yeyote mbali na afisa wa serikali anayeshikilia afisi ya umma.

”afisi ya umma” inamaanisha afisi katika serikali ya kitaifa, serikali ya kaunti au katika huduma za umma, iwapo zawadi na faida za afisi hulipwa kutoka katika Mfuko wa Jumla au moja kwa moja kutoka kwa pesa zinazotolewa na Bunge.

“huduma ya umma” inamaanisha watu wote kwa pamoja, mbali na maafisa wa serikali, wanaofanya kazi katika idara ya Serikali;

“jamhuri” inamaanisha Jamhuri ya Kenya;

“serikali” inapotumiwa kama nomino, ina maana ya mseto wa afisa, idara na asasi zingine zinazounda serikali ya Jamhuri chini ya Katiba hii;

“afisi ya serikali” inamaanisha yoyote katika hizi–

 • (a) Rais;
 • (b) Naibu wa Rais;
 • (c) Waziri;
 • (d) Mbunge;
 • (e) Majaji na Mahakimu;
 • (f) Mwanachama wa Tume chini ya Sura ya Kumi na tano;
 • (g) Anayeshikilia wadhifa wa afisi huru chini ya Sura ya Kumi na tano;
 • (h) Mwanachama wa baraza la kaunti, gavana au naibu wa gavana wa kaunti, au mwanachama yeyote wa mamlaka kuu ya kaunti;
 • (i) Mwanasheria Mkuu;
 • (j) Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma;
 • (k) Katibu wa Baraza la Mawaziri;
 • (l) Katibu Mkuu;
 • (m)Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi;
 • (n) Kamanda wa huduma ya Majeshi ya Ulinzi ya Kenya;
 • (o) Mkurugenzi-Mkuu wa Huduma za Kitaifa za Upelelezi;
 • (p) Inspekta-Mkuu, na Naibu wa Inspekta-Mkuu, wa Huduma za Polisi za Kitaifa; au
 • (q) afisi ambayo imeundwa na kuchukuliwa kama afisi ya serikali chini ya sheria ya kitaifa;

“afisa wa serikali” inamaanisha mtu anayeshikilia afisi ya Kitaifa;

“idara ya Serikali” inamaanisha Tume, afisi, shirika au asasi nyingine iliyoundwa chini ya Katiba hii;

“Maandishi” inahusisha upigaji chapa, upigaji picha, lithografia, upigaji taipu, breli na njia yoyote nyingine inayowakilisha au kuzalisha maneno kwa njia inayoonekana; na

“vijana” inamaanisha ujumla wa watu wote katika Jamhuri ambao–

 • (a) wametimiza umri wa miaka kumi na minane; lakini
 • (b) hawajatimiza umri wa miaka thelathini na mitano.