Ruka hadi Yaliyomo

Kifungu 259. Kufasiri Katiba Hii

(1) Katiba hii itafasiriwa kwa namna ambayo–

 • (a) inakuza malengo, maadili na kanuni zake;
 • (b) inaendeleza utawala wa sheria, haki za binadamu na uhuru wa kimsingi ulioko katika Sheria ya Haki;
 • (c) inaruhusu maendeleo ya sheria; na
 • (d) inachangia utawala bora.

(2) Iwapo kuna mkinzano kati ya matoleo ya lugha tofauti ya Katiba hii, toleo la lugha ya Kiingereza ndilo litakalotawala.

(3) kila sharti la Katiba hii litafasiriwa kulingana na kanuni za ufasiri kwamba sheria kila mara inazungumza, na hivyo basi, miongoni mwa vitu vingine–

 • (a) jukumu la mamlaka lililotolewa na Katiba hii kwa afisi linaweza kufanywa au kutekelezwa na mtu anayeshikilia wadhifa katika afisi hiyo kama inavyohitajika;
 • (b) rejeleo lolote katika Katiba hii kwa serikali au kwa afisi nyingine ya umma au afisa, au mtu anayeshilikia afisi hiyo ni rejeleo kwa mtu anayeshikilia afisi hiyo kwa muda au anayetekeleza majukumu ya afisi hiyo wakati wowote ule;
 • (c) rejeleo katika Katiba hii kwa afisi, idara ya serikali au mahali palipotajwa kwenye Katiba hii litasomwa pamoja na badiliko lolote rasmi linalohitajika ili likubalike katika mazingira hayo; na
 • (d) rejeleo katika Katiba hii kwa afisi, kundi au shirika, ikiwa ni afisi, na iwapo kundi au shirika halipo tena, basi yule aliyerithi ndiye atakayerejelewa au yeyote husika katika afisi, kundi au shirika.

(4) Katika Katiba hii, isipokuwa pale ambapo muktadha unahitaji vinginevyo–

 • (a) iwapo neno au maelezo yamefafanuliwa katika Katiba hii, tofauti zozote za kisarufi au matumizi ya neno linalohusiana na jingine, soma ukizingatia mabadiliko yanayotokana na muktadha; na
 • (b) neno “-kiwemo” linamaanisha “ikiwemo, lakini bila mpaka”.

(5) Katika kuhesabu wakati baina ya matukio mawili kwa shughuli yoyote katika Katiba hii, kama wakati umeelezwa–

 • (a) kama siku, basi siku ambayo tukio la kwanza linatokea haitazingatiwa, na siku ambayo tukio la mwisho linaweza kutokea itahusishwa;
 • (b) kama miezi, kipindi cha muda uliowekwa huisha mwanzoni mwa siku katika mwezi husika-
  • (i) ambao una nambari sawa kama tarehe ambapo kipindi hicho kilianza, iwapo mwezi huo una tarehe inayolingana; au
  • (ii) hiyo ndiyo siku ya mwisho ya mwezi huo; au
 • (c) kama miaka, kipindi cha muda huo kinamalizika mwanzoni mwa tarehe ya mwaka husika inayolingana na tarehe ambayo kipindi hicho kilianza.

(6) Iwapo muda uliotengwa katika Katiba hii kwa lengo lolote ni siku sita au chini yake, Jumapili na siku za mapumziko hazitahesabiwa wakati wa kuhesabu muda.

(7) Iwapo, katika hali yoyote maalumu, kipindi cha muda kilichoelezwa na Katiba hii kinakamilika Jumapili au siku ya mapumziko, muda huo unaongezwa hadi siku inayofuata ambayo siyo Jumapili au siku ya mapumziko.

(8) Iwapo muda fulani haukuelezwa na Katiba hii ili kuekeleza kitendo fulani, kitendo hicho kitafanywa bila kuchelewa na kulingana na wakati wowote shughuli hiyo inapohitajika.

(9) Iwapo mtu yeyote au idara ya Serikali ina mamlaka chini ya Katiba hii kuongeza kipindi cha muda unaoruhusiwa katika Katiba hii, mamlaka hayo yanaweza kutekelezwa kabla au baada ya mwisho wa kipindi hicho isipokuwa pale ambapo nia tofauti imeelezwa wazi katika sharti linalotoa mamlaka hayo.

(10) Isipokuwa pale ambapo Katiba hii inaeleza tofauti, ikiwa mtu ameondoka katika afisi iliyoundwa na Katiba hii, iwapo mtu huyo anastahili kutokana na umahiri wake kazini, anaweza kuteuliwa tena, kuchaguliwa kwa kupigiwa kura au vinginevyo kuchaguliwa tu kuchukua afisi hiyo kulingana na Katiba hii.

(11) Ikiwa jukumu au mamlaka yaliyopewa mtu chini ya Katiba hii hutekelezwa na mtu huyo tu kupitia kwa ushauri au pendekezo, kupitia mwingine, jukumu linaweza kufanywa ama mamlaka kutekelezwa kupitia tu kwa ushauri huo, pendekezo, kwa kuidhinisha au kukubali huko, au baada ya mashauriano hayo, isipokuwa pale ambapo Katiba hii inaeleza vinginevyo.