Ruka hadi Yaliyomo
AfroCave

Kifungu 257. Marekebisho Yanayotokana na Juhudi za Wengi

(1) Marekebisho ya Katiba hii yanaweza kupendekezwa kutokana na juhudi za wengi ikiwa angalau watu milioni moja waliojiandikisha kupiga kura wametia sahihi.

(2) Juhudi za wengi za marekebisho ya Katiba hii zinaweza kuchukua muundo wa pendekezo la jumla au kupitia kwa rasimu ya Mswada iliyotayarishwa.

(3) juhudi za wengi zitahusisha kupitia kwa njia ya pendekezo la jumla, wanaoendeleza pendekezo hili watalitayarisha liwe kama rasimu ya Mswada kupitia kwa wadhamini wao.

(4) Wadhamini wanaoendeleza juhudi za wengi watawasilisha rasimu ya Mswada pamoja na sahihi walizokusanya kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ambayo itathibitisha kwamba pendekezo hilo linaungwa mkono na angalau na wapiga kura milioni moja waliosajiliwa.

(5) Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka itakaporidhika kwamba pendekezo hilo limetimiza masharti ya Kifungu hiki, Tume hii itawasilisha pendekezo hilo kwa kila baraza la kaunti ili kujadiliwa katika muda wa miezi mitatu baada ya tarehe ya kuwasilishwa na Tume hiyo.

(6) Iwapo baraza la kaunti litaidhinisha rasimu ya Mswada katika kipindi cha miezi mitatu tangu tarehe ilipowasilishwa na Tume, Spika wa baraza la kaunti atawasilisha nakala ya rasimu ya Mswada kwa Maspika wawili wa viwango vyote viwili vya Bunge, pamoja na cheti kwamba baraza la kaunti limeidhinisha.

(7) Iwapo rasimu ya Mswada imeidhinishwa na mabaraza mengi ya kaunti, rasimu hiyo itawasilishwa Bungeni bila kuchelewa.

(8) Chini ya kifungu hiki, Mswada utaidhinishwa na Bunge iwapo utaungwa mkono na wabunge wengi katika kila kiwango cha Bunge.

(9) Iwapo Bunge litaupitisha Mswada huo, utapelekewa Rais kutiwa sahihi kulingana na Kifungu cha 256 (4) na (5).

(10) Iwapo kila ngazi ya Bunge haitapitisha Mswada, au Mswada huo unahusu suala lililotajwa katika kifungu cha 255 (1), Mswada huo uliopendekezwa utapalekwa kwa watu kwa kura ya maamuzi

(11) Kifungu cha 255 (2) kitatumika, kukiwemo na marekebisho muhimu yoyote, katika kura ya maamuzi chini ya ibara ya (10).