Ruka hadi Yaliyomo
AfroCave

Kifungu 94. Jukumu la Bunge

(1) Mamlaka ya utungaji wa sheria ya Jamhuri hii inatokana na wananchi na katika kiwango cha kitaifa, yamekabidhiwa kwa na kutekelezwa na Bunge.

(2) Bunge hufuatilia uanuwai wa taifa, huwakilisha nia ya wananchi, na hutekeleza Mamlaka yao.

(3) Bunge linaweza kukubali na kupitisha marekebisho kwenye Katiba hii na kubadilisha mipaka ya kaunti kama inavyoagizwa katika Katiba hii;

(4) Bunge litalinda Katiba hii na kudumisha utawala wa kidemokrasia katika Jamhuri hii.

(5) Hakuna mtu yeyote au asasi yoyote, isipokuwa Bunge, itakayokuwa na mamlaka ya kuunda masharti yatakayokuwa na nguvu za kisheria nchini Kenya isipokuwa kwa amri ya Katiba hii iliyokabidhiwa Bunge au kwa Sheria ya Bunge.

(6) Sheria ya Bunge, au sheria ya kaunti, inayoipatia asasi yoyote ya Serikali, afisa wa Serikali, au mtu yeyote mamlaka ya kutunga masharti au sheria na kuipatia nguvu za kisheria nchini Kenya, kama inavyokusudiwa katika Ibara ya (5), itaeleza bayana na kwa hakika shabaha na malengo ya kukabidhiwa mamlaka haya, viwango vya mamlaka, hali na upeo wa sheria zitakavyotungwa, na kanuni na viwango vya ubora vinavyotumika kisheria na vilivyobuniwa chini ya mamlaka haya.