Ruka hadi Yaliyomo
AfroCave

Kifungu 245. Uongozi Katika Huduma za Polisi za Kitaifa

(1) Afisi ya Inspekta-Mkuu wa Huduma za Polisi za Kitaifa imeundwa.

(2) Inspekta-Mkuu–

 • (a) atateuliwa na Rais kwa idhini ya Bunge; na
 • (b) atakuwa na mamlaka huru ya kuongoza Huduma za Polisi za Kitaifa na kutekeleza majukumu mengine yoyote kwa mujibu wa sheria ya nchi.

(3) Huduma za Polisi na Huduma za Polisi wa Utawala, kila kimoja katika vikosi hivi kitaongozwa na Naibu Inspekta-Mkuu atakayeteuliwa na Rais kulingana na mapendekezo ya Tume ya Huduma za Polisi za Kitaifa.

(4) Waziri anayehusika na huduma za polisi anaweza kutoa agizo kisheria kwa InspektaMkuu kuhusu suala lolote la sera kwa Huduma za Polisi za Kitaifa; lakini hakuna mtu yeyote atakayetoa agizo kwa Inspekta-Mkuu kuhusiana na–

 • (a) upelelezi wa kosa fulani au makosa fulani;
 • (b) utekelezaji wa sheria dhidi ya mtu au watu; au
 • (c) kuajiri, kutoa majukumu, kupandisha cheo, kusimamisha au kufuta kazi kwa mfanyakazi yeyote wa Huduma za Polisi za Kitaifa.

(5) Agizo lolote linalotolewa kwa Inspekta-Mkuu na Waziri anayehusika na huduma za polisi chini ya ibara ya (4), au agizo lolote analopewa Inspekta-Mkuu na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma chini ya kifungu cha 157(4), litakuwa kwa maandishi.

(6) Inspekta-Mkuu atahudumu katika wadhifa huo kwa kipindi kimoja cha miaka minne na hatateuliwa tena kwa kipindi kingine.

(7) Inspekta-Mkuu huweza kuondolewa mamlakani na Rais lakini kwa sababu ya–

 • (a) kukiuka Katiba hii au sheria nyingine yoyote, pamoja na kukiuka sura ya sita;
 • (b) utovu wa nidhamu ama katika utekelezaji wa majukumu ya kiafisi au vinginevyo;
 • (c) kutokuwa na uwezo wa kimwili au kiakili utakaomzuia kutekeleza majukumu ya afisi yake;
 • (d) kushindwa kutekeleza majukumu yake;
 • (e) kufilisika; au
 • (f) sababu nyingine yoyote inayoridhisha.

(8) Bunge litatunga sheria itakayoidhinisha kutekelezwa kikamilifu kwa Kifungu hiki.