Ruka hadi Yaliyomo
AfroCave

Utaratibu wa Kutunga Sheria katika Baraza la Kaunti

  • Mwandishi Gĩthĩnji
  • Imesasishwa:

Utaratibu wa kutunga sheria katika Baraza la Kaunti nchini Kenya unahusisha hatua kadhaa, kuanzia Hatua ya Kwanza hadi kuidhinishwa na Gavana wa Kaunti.

Kifungu cha 1 cha Katiba kinakabidhi mamlaka ya watu kwa Baraza za Kaunti, miongoni mwa tume zingine huru.

Mswada, kwa madhumini ya makala haya, ni pendekezo la sheria mpya, au pendekezo la kubadilisha sheria iliyopo, uliowasilishwa kwa mjadala mbele ya Baraza la Kaunti.

Jedwali la YaliyomoOnyesha/Ficha

Asili ya Miswada Katika Kiwango cha Kaunti

Mswada unaweza kutoka kwa–

  • chama cha kisiasa - uliowasilishwa katika Baraza la Kaunti kwa jina la Kiongozi wa Chama cha Walio wengi au Kiongozi wa Chama cha Wachache, au manaibu wao;
  • Kamati ya Mamlaka Kuu ya Kaunti - uliowasilishwa kwa jina la Kiongozi wa Chama cha Walio Wengi au Kiongozi wa Chama cha Wachache, au kwa jina la Mwenyekiti wa kamati husika;
  • wanachama binafsi wa Baraza la Kaunti - uliowasilishwa kwa jina la mwanachama anayefadhili Mswada huo;
  • Kamati ya Baraza la Kaunti - uliowasilishwa kwa jina la Mwenyekiti au mwanachama aliyeteuliwa na Kamati;
  • mwananchi pia anaweza kuwasilisha maombi kwa Baraza la Kaunti kutunga sheria kuhusu jambo fulani, kulingana na Sehemu ya 15 ya Sheria ya Serikali za Kaunti na Kanuni za Kudumu za Baraza la Kaunti - uliowasilishwa kwa njia ya maombi kupitia kwa Spika wa Baraza la Kaunti na kukabidhiwa kwa Kamati ya Idara inayohusika kwa ajili ya kuzingatiwa na kuchapishwa kwa Mswada unaofuata ombi hilo;
  • kwa upande mwingine, wananchi wanaweza kupeleka mapendekezo ya kisheria kwa Wanachama wa Baraza la Kaunti.

Utaratibu wa Kutunga Sheria katika Baraza la Kaunti

Utaratibu wa kutunga sheria katika Baraza la Kaunti huchukua hatua kadhaa ambapo Mswada hupitishwa katika Baraza hilo baada ya kuchapishwa kwake.

Usomaji wa Kwanza

Usomaji wa Kwanza wa Mswada huhusisha Karani wa Baraza la Kaunti kuwasilisha Mswada huo mbele ya Baraza hilo kwa mara ya kwanza kwa kusoma kichwa chake. Hatua hii ni ya utaratibu tu na hakuna kupiga kura au kutokea kwa mjadala wowote.

Mswada huo hupewa nambari ya ufuatiliaji na kisha kukabidhiwa kwa Kamati ya Idara ya Baraza husika kwa ajili ya kuzingatiwa.

Kamati husika kisha huwezesha ushiriki wa umma kwa njia zinazofaa kama vile–

  • kukaribisha kuwasilisha memoranda;
  • kufanya mikutano ya hadhara;
  • kushauriana na wadau husika; na
  • kutafuta ushauri wa wataalam juu ya masuala ya kiufundi.

Kamati husika huyazingatia maoni na mapendekezo ya wananchi wakati wa kuzingatia Mswada na kuandaa taarifa yake kwa .Baraza

Kamati husika inauchambua Mswada huo kwa kumwita mfadhili wa Mswada huo, na kuwaalika wadau mbalimbali na baadaye kuandaa taarifa ya Baraza pamoja na mapendekezo ya marekebisho yoyote ambayo Kamati ya Baraza zima itazingatia baadaye.

Usomaji wa Pili

Usomaji wa Pili wa Mswada ni hatua ya kutunga sheria ya Baraza la Kaunti ambapo rasimu ya Mswada husoma kwa mara ya pili.

Wanachama wa Baraza la Kaunti hujadili madhumuni na kanuni kuu za Mswada huo wakiwa katika kikao cha jumla. Wwanachama anayefadhili Mswada hufungua mjadala wa Usomaji wa Pili kwa kuweka hoja ya Mswada na kueleza masharti yake, huku mwanachama mwingine akiuunga mkono. Mswada ambao haujaungwa mkono huondolewa.

Majadiliano yanahusu vipengele vyote vya Mswada, ikijumuisha malengo yake, kanuni, na jinsi kupitishwa kwake kutakavyoathiri umma kwa ujumla.

Ripoti ya Kamati ya Idara Husika huwasaidia wanachama kujadili Mswada huo, haswa kufahamu maoni ya umma au adhari za Mswada huo kwa sheria nyinginezo.

Asili ya Mswada huamua hatua yake ya mjadala, kuanzia saa chache hadi siku kadhaa za kikao cha Baraza la Kaunti.

Spika wa Baraza la Kaunti humruhusu mpendekezaji wa Mswada kujibu maswala yoyote yaliyotolewa na Baraza la Kaunti baada ya mjadala. Kisha Spika anauliza swali, na kusababisha Baraza kupiga kura ya iwapo Mswada huo uende katika hatua inayofuata au la.

Hakuna marekebisho yanayoweza kufanywa kwa (maandishi ya) Mswada katika hatua hii, ingawa wanachama wanaweza kutoa wazo la mabadiliko watakayopendekeza baadaye.

Hatua ya Kamati

Hatua hii inafanyika kupitia Kamati ya Baraza zima. Hatua ya kamati inajumuisha uchunguzi wa makini (mstari kwa mstari) wa sehemu nyingi za Mswada (vifungu) na upigaji kura wa wanachama wa Kamati juu ya kila marekebisho.

Kamati ya Baraza zima inajumuisha wanachama wote wa Baraza walioketi kwa namna ya kamati, ambao Naibu Spika au mwanachama yeyote wa jopo la Wenyeviti anaongoza.

Kamati hiyo huamua iwapo kila kifungu cha Mswada kibaki ndani yake. Kila kifungu katika Mswada kinakubaliwa, kubadilishwa au kuondolewa.

Vifungu na ratiba za Mswada huidhinishwa na Kamati ya Baraza zima, pamoja na marekebisho au bila marekebisho. Baada ya kumalizika kwa kikao hicho, Kamati kupitia Mwenyekiti wake huwasilisha taarifa kwenye Baraza kwa ajili ya kuidhinishwa.

Marekebisho hayo yanaweza kupendekeza mabadiliko mapya kwa masharti yaliyopo ya Mswada au kujumuisha mengine mapya. Hata hivyo, yanapoanzishwa, marekebisho yanapaswa kuwa karibu na mada ya Mswada.

Mswada katika hatua ya kamati (na hatua nyingine) unaweza kujumuisha marekebisho ili kuhakikisha Mswada huo unafanya kazi kama ilivyokusudiwa, kutekeleza sera mpya, au kuwa marekebisho ya maelewano ili kuufanya Mswada huo kudhibitiwa zaidi.

Marekebisho ya maelewano yanajibu hoja zilizotolewa katika hatua ya awali au yanawasilishwa ili kuepusha kushindwa kwa serikali katika hatua inayohusika.

Hatua ya Ripoti

Hatua hii inafanyika katika ukumbi wa Baraza la Kaunti wakati wa kikao cha jumla. Baraza linajadili tu marekebisho katika hatua hii.

Baraza linapokea ripoti na kuipigia kura kufuatia Hoja ya kiutaratibu. Katika hatua hii, Wwanachama yeyote anaweza, kwa sababu, pia kulipendekeza Baraza lijiamulie kuwa Kamati tena ili kupitia upya vifungu vyovyote vilivyoainishwa vya Mswada huo.

Marekebisho yanaweza kubadilisha kile kilicho kwenye Mswada tayari au yanaweza kuhusisha masharti mapya kuongezwa.

Usomaji wa Tatu

Somo la tatu la Mswada linahusisha mjadala wa jumla wa Mswada mara baada ya Hatua ya Ripoti. Marekebisho (mapendekezo ya mabadiliko) hayawezi kufanywa kwa Mswada katika usomaji wa tatu, ingawa kuyasafisha marekebisho kunaweza kukubalika.

Kusafisha Mswada (kutayarisha marekebisho na kuorodheshwa upya kwa vifungu) huhakikisha sheria ya baadaye ni ya ufanisi na inayotekelezeka (bila mianya).

Mjadala kwa kawaida huwa mfupi na unahusisha tu kile ambacho kipo kwenye Mswada, badala ya kile ambacho kingeweza kujumuishwa, kama katika Somo la Pili.

Mwishoni mwa mjadala, Baraza la Kaunti litapiga kura ya mwisho kuhusu Mswada, yaani, linaamua (kwa kupiga kura) iwapo litaidhinisha Mswada huo kusomwa mara ya tatu.

Idhini ya Gavana wa Kaunti

Pindi Baraza la Kaunti linapopitisha Mswada, Spika anauwasilisha kwa Gavana wa Kaunti ambaye, ndani ya siku kumi na nne, anaweza-

  • kutia saini Mswada huo; au
  • kuurejesha Mswada kwa Baraza la Kaunti na hati ya kutoridhishwa.

Ikiwa Gavana wa Kaunti ataidhinisha Mswada, unakuwa sheria.

Katika hali fulani, sheria haiwezi kuanza kutumika mara moja na tarehe ya kuanza inaweza kuonyeshwa (kama tarehe ya baadaye). Hii inaruhusu serikali ya kaunti kupanga ipasavyo, kama vile kuandaa kanuni zinazojaza maelezo ya sheria mpya.

Kurejeshwa kwa Mswada kwa Baraza la Kaunti

Iwapo Gavana wa Kaunti atarejesha Mswada kwa Baraza la Kaunti, Baraza hilo linapaswa kutafakari upya Mswada huo, likijihusisha tu na vipengee ambavyo Gavana wa Kaunti alieleza kutoridhishwa kwake, ikijumuisha mapendekezo yoyote ambayo Gavana wa Kaunti anaweza kutoa kuhusu vipengee hivyo, na-

  • Baraza la Kaunti linaweza kurekebisha Mswada huo kwa kuzingatia sababu za kutoridhishwa kwa Gavana wa Kaunti au kupitisha Mswada huo mara ya Pili bila marekebisho. Iwapo Baraza litapitisha Mswada unaoshughulikia kikamilifu sababu za kutoridhishwa kwa Gavana wa Kaunti, Spika wa Baraza la Kaunti atawasilisha Mswada huo kwa Gavana wa Kaunti ili aidhinishwe;
  • Baraza linaweza kupitisha Mswada huo mara ya pili na–
    • kusisitiza maandishi yake ya awali bila kujali sababu za kutoridhishwa kwa Gavana wa Kaunti; au
    • kupitisha Mswada kwa mara ya pili na marekebisho ambayo hayatoshelezi kikamilifu sababu za kutoridhishwa kwa Gavana wa Kaunti.
      mifano yote miwili iinahitaji kura ya thuluthi mbili ya Baraza la Kaunti. Baada ya hapo, Spika anawasilisha Mswada tena kwa Gavana wa Kaunti ili uidhinishwe.
Makala Zaidi