Ruka hadi Yaliyomo
AfroCave

Kifungu 152. Baraza la Mawaziri

(1) Baraza la Mawaziri litakuwa na–

 • (a) Rais;
 • (b) Naibu wa rais;
 • (c) Mwanasheria Mkuu;
 • (d) Mawaziri wasiopungua kumi na wanne au kuzidi ishirini na wawili;

(2) Rais atawapendekeza na kwa idhini ya Baraza la Kitaifa kuwateua Mawaziri.

(3) Waziri hatakuwa Mbunge.

(4) Kila mtu atakayeteuliwa kama waziri–

 • (a) atachukua mamlaka kwa kuapa au kukiri kwa watu na Jamhuri ya Kenya na kutii Katiba, mbele ya Rais na kwa mujibu wa Ratiba ya Nne; na
 • (b) anaweza kujiuzulu kwa kuwasilisha kwa Rais taarifa iliyoandikwa ya kujiuzulu kwake.

(5) Rais–

 • (a) anaweza kubadilisha kazi ya Waziri;
 • (b) anaweza kumwachiza kazi Waziri; na
 • (c) atamwachisha kazi waziri iwapo itahitajika kufanya hivyo, kwa uamuzi unaochukuliwa chini ya ibara ya (6) hadi (10).

(6) Mwanachama wa Baraza la Kitaifa anayeungwa mkono na angalau robo moja ya wabunge wote, anaweza kupendekeza mjadala wa kumtaka Rais amwachishe kazi waziri–

 • (a) kwa misingi ya kukiuka kwa hali ya juu Vifungu vya Katiba hii au sheria nyingine yoyote;
 • (b) kwa kuwa kuna sababu kali za kuamini kwamba Waziri amefanya kosa la jinai chini ya sheria za kitaifa na kimataifa; au
 • (c) kwa kuwa na utovu wa nidhamu wa hali ya juu.

(7) Iwapo mjadala chini ya ibara ya (5) utaungwa mkono na angalau thuluthi moja ya wabunge wote wa Baraza la Kitaifa–

 • (a) Bunge litateua kamati maalumu itakayokuwa na wanachama kumi na mmoja kuchunguza suala hili; na
 • (b) katika muda wa siku kumi, kamati hii maalumu itaripoti kwa Baraza la Kitaifa ikiwa limepata iwapo madai dhidi ya Waziri ni ya kuthibitika.

(8) Waziri ana haki ya kwenda au kuwakilishwa mbele ya kamati maalumu wakati wa uchunguzi wake.

(9) Iwapo kamati maalumu itaripoti kwamba imepata madai–

 • (a) hayathibitiki, hakuna taratibu nyingine zitakazochukuliwa; ama
 • (b) yamethibitika, Baraza la Kitaifa-
  • (i) litampa Waziri nafasi ya kusikizwa; na
  • (ii) litapiga kura kama litaidhinisha uamuzi unaomtaka Waziri kuachishwa kazi.

(10) Iwapo uamuzi ulio chini ya ibara ya (8) unaomtaka Rais kumwachiza kazi Waziri, utaungwa mkono na wingi wa wabunge wa Baraza la Kitaifa–

 • (a) Spika kwa haraka atawasilisha uamuzi huu kwa Rais; na
 • (b) Rais atamwachisha kazi waziri.