Ruka hadi Yaliyomo
AfroCave

Kifungu 138. Tararatibu Katika Uchaguzi wa Rais

(1) Iwapo ni mgombea urais mmoja tu atateuliwa, mgombeaji huyoatatangazwa kuwa ameteuliwa.

(2) Iwapo wagombeaji wa urais wawili au zaidi watateuliwa, uchaguzi wa urais utafanyika katika kila eneobunge.

(3) Katika uchaguzi wa urais–

  • (a) wapigakura wote waliosajiliwa kama wapigakura kwa kusudi la uchaguzi wa wabunge wana haki ya kupiga kura.
  • (b) uchaguzi utakuwa kwa njia ya siri katika siku ambayo imeelezewa kwenye ibara ya 101(1) na kwa wakati, mahali na kwa njia ambayo imeamriwa chini ya Sheria ya Bunge; na
  • (c) baada ya kuhesabiwa kwa kura katika vituo vya kupigia kura, Tume Huru ya Uchaguzi na mipaka itahesabu na kuhakikisha hesabu ya kura na kutangaza matokeo.

(4) Mgombea urais atatangazwa kuwa Rais iwapo atapokea–

  • (a) zaidi ya nusu ya kura zote zilizopigwa katika uchaguzi; na
  • (b) angalau asilimia ishirini na tano ya kura zilizopigwa katika kila kaunti na kaunti ziwe zaidi ya nusu ya kaunti zote kwa jumla.

(5) Iwapo hakuna mgombeaji amechaguliwa, uchaguzi mwingine utafanyika upya katika kipindi cha siku thelathini baada ya uchaguzi uliopita, na katika uchaguzi huo mpya, wagombeji watakuwa–

  • (a) mgombeaji au wagombeaji ambao walipata kura nyingi zaidi; na
  • (b) mgombeaji au wagombeaji ambao walipata idadi ya pili ya wingi wa kura.

(6) pale ambapo wagombeaji zaidi ya mmoja wamepata idadi kubwa zaidi ya kura, ibara ya (5) (b) haitatumika na wagombeaji pekee katika uchaguzi mpya watakuwa wale ambao wameelezewa katika Ibara ya (5) (a).

(7) Mgombeaji ambaye atapata idadi kubwa zaidi ya kura kwenye uchaguzi mpya, atatangazwa kuwa Rais.

(8) Uchaguzi wa urais utafutiliwa mbali na uchaguzi mwingine mpya kufanyika iwapo–

  • (a) hakuna mtu ambaye ameteuliwa kama mgombea uchaguzi kabla ya kumalizika kwa kipindi kilichowekwa cha kuwasilisha watakaoteuliwa;
  • (b) mgombea uchaguzi wa urais au naibu wa Rais ataaga dunia mnamo au kabla ya tarehe iliyopangiwa kufanyika uchaguzi ;au
  • (c) mgombea uchaguzi ambaye alistahili kutangazwa kuwa Rais, kuaga dunia kabla ya kutangazwa kama Rais.

(9) Uchaguzi mpya wa urais chini ya ibara ya (8) utafanyika katika muda wa siku sitini baada ya tarehe iliyokuwa imewekwa ya uchaguzi uliotangulia.

(10) Katika muda wa siku saba baada uchaguzi wa urais, mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka–

  • (a) atangaza matokeo ya uchaguzi; na
  • (b) atawasilisha ripoti iliyoandikwa ya matokeo ya uchaguzi kwa Jaji Mkuu na Rais aliye mamlakani.