Ruka hadi Yaliyomo
AfroCave

Kifungu 123. Maamuzi ya Seneti

(1) Kwa uchaguzi, wanachama wote wa Seneti ambao walikuwa wameandikishwa kama wapigakura katika kaunti fulani, kwa pamoja wataunda ujumbe mmoja kwa lengo la Ibara ya (4) na mwanachama aliyechaguliwa chini ya Kifungu cha (98) (1) (a) atakuwa ndiye kiongozi wa ujumbe huo.

(2) Wakati Seneti itakapopigia kura kuhusiana na suala lolote isipokowa Mswada, Spika ataamua iwapo suala hilo linaathiri au kutoathiri kaunti.

(3) Seneti inapopiga kura kuhusu suala ambalo haliathiri kaunti, kila Seneta atakuwa na kura moja.

(4) Isipokuwa iwe vinginevyo, kama inavyoagizwa na Katiba hii, kwa suala lolote katika Seneti linaloathiri kaunti–

  • (a) kila ujumbe wa kaunti utakuwa na kura moja itakayopigwa na kiongozi wa ujumbe wa kaunti kwa niaba ya kaunti au, endapo hakuna kiongozi wa ujumbe huo, basi ipigwe na mwanachama mmoja wa ujumbe huo aliyeteuliwa na kiongozi wa ujumbe huo.
  • (b ) mtu ambaye anapiga kura kwa niaba ya ujumbe ataamua iwapo apige kura kwa kuunga mkono au kinyume cha suala hilo, baada ya kushauriana na wajumbe; au (c) suala hilo litaendelezwa iwapo litaungwa mkono na wajumbe walio wengi.