Ruka hadi Yaliyomo
AfroCave

Kifungu 67. Tume ya Kitaifa ya Ardhi

(1) Tume ya Kitaifa ya Ardhi imeundwa.

(2) Majukumu ya Tume ya Kitaifa ya Ardhi ni–

  • (a) kusimamia ardhi ya umma kwa niaba ya Serikali ya kitaifa na kaunti;
  • (b) kupendekezea Serikali ya kitaifa sera ya kitaifa kuhusu ardhi;
  • (c) kushauri Serikali ya kitaifa kuhusu utaratibu wa kina wa kusajili umiliki wa ardhi kote nchini.
  • (d) kufanya utafiti kuhusiana na ardhi na matumizi ya rasilmali nyingine za kiasili na kutoa mapendekezo kwa mamlaka yanayohusika;
  • (e) kuanzisha uchunguzi wake au kutokana na malalamiko kuhusu ukiuakaji haki uliopo au wa kihistoria kuhusu ardhi na kupendekeza suluhisho mwafaka;
  • (f) kuhimiza matumizi ya njia za kiasili zinazokubalika za kusuluhisha mizozo inayohusu ardhi;
  • (g) kutathmini ushuru unaotozwa ardhi na thamani ya mali isiyoweza kuhamishwa katika eneo lolote linalotambuliwa na sheria;
  • (h) kusimamia na kuwa na jukumu la kuangalia mpango wa matumizi ya ardhi nchini;

(3) Tume ya Kitaifa ya Ardhi inaweza kutekeleza majukumu mengine yatakayotolewa na sheria ya nchi.