Ruka hadi Yaliyomo
AfroCave

Kifungu 63. Ardhi ya Jamii

(1) Ardhi ya jamii itatolewa na kumilikiwa na jamii zinazotambuliwa kwa misingi ya kikabila, kitamaduni au mahitaji ya kijamii yanayofanana.

(2) Ardhi ya jamii inahusisha–

  • (a) ardhi iliyosajiliwa kwa jina la wawakilishi wa kikundi kilicho chini ya masharti ya sheria yoyote;
  • (b) ardhi yoyote iliyokabidhiwa jamii fulani kupitia kwa njia yoyote ya kisheria;
  • (c) ardhi nyingine yoyote itakayotangazwa na Sheria ya Bunge kama ardhi ya jamii; na
  • (d) ardhi ambayo–
    • (i) inamilikiwa kihalali , kusimamiwa au kutumiwa na jamii maalum kama misitu ya jamii, malisho ya mifugo au madhabahu;
    • (ii) ardhi ya kinasaba na ardhi ambayo kitamaduni ilimilikiwa na jamii ya wawindaji; au
    • (iii) kisheria inashikiliwa kama ardhi ya amana na serikali za Kaunti lakini isiyojumuisha ardhi ya umma iliyoshikiliwa kama amana na serikali za kaunti chini ya Kifungu cha 62 (2).

(3) Ardhi yoyote ya jamii ambayo haijasajiliwa itashikiliwa kwa amana na Serikali za kaunti kwa niaba ya jamii hizo.

(4) Ardhi ya jamii haitatolewa au kutumiwa vinginevyo isipokuwa kwa misingi ya sheria inayofafanua hali na viwango vya haki za kila mwanajamii kibinafsi au wanajamii wote kwa pamoja.

(5) Bunge litatunga sheria kuidhinisha utekelezwaji wa Kifungu hiki.