Ruka hadi Yaliyomo
AfroCave

Kifungu 53. Watoto

(1) Kila mtoto ana haki ya–

  • (a) jina na uraia kuanzia anapozaliwa;
  • (b) elimu ya msingi bila malipo na ya lazima;
  • (c) Lishe bora ya kimsingi, makazi na huduma za afya;
  • (d) kulindwa dhidi ya kutumiwa vibaya, kutelekezwa, tamaduni za kuumiza, aina zozote za ghasia, matendo na adhabu zisizo za kibinadamu, kutumiwa vibaya, na kazi yoyote ya kunyanyasa au ya kuhatarisha;
  • (e) kutunzwa na kulindwa na wazazi, ambayo inahusu wajibu sawa kutoka kwa mama na baba wa kumkimu mtoto, iwe wameoana au la; na
  • (f) kutofungwa kinyume na matakwa yake isipokuwa endapo hiyo ndiyo hatua ya mwisho, na wakizuiliwa–
    • (i) kuzuiliwa kwa muda mfupi na unaostahili tu; na
    • (ii) kutenganishwa na watu wazima katika jela huku ikizingatiwa umri na jinsia ya mtoto.

(2) Maslahi ya mtoto ni muhimu sana katika kila suala linalomhusu mtoto.