Ruka hadi Yaliyomo
AfroCave

Kifungu 40. Ulinzi wa Haki ya Kumiliki Mali

(1) Kwa kuzingatia Kifungu cha 65, kila mtu ana haki, kibinafsi au kwa kuungana na wengine kupata na kumiliki mali–

  • (a) ya aina yoyote; na
  • (b) katika sehemu yoyote ya Kenya.

(2) Bunge halitatunga sheria inayoruhusu Serikali au mtu yeyote–

  • (a) kidhalimu kumpokonya mtu mali ya aina yoyote, au thamana ama haki juu ya, mali ya aina yoyote;
  • (b) kumzuia, au kwa njia yoyote kumnyima kufurahia haki chini ya Kifungu hiki katika misingi iliyobainishwa katika Kifungu cha (27) (4).

(3) Serikali haitamnyima mtu yeyote haki ya kuwa na mali ya aina yoyote, au nia au haki ya kuwa na mali ya aina yoyote isipokuwa endapo kuzuiwa huko–

  • (a) kunatokana na upataji ardhi au nia ya kutaka ardhi au kubadilisha maslahi fulani ili kupata ardhi, au hatimiliki ya ardhi, kwa mujibu wa Sura ya Tano; au
  • (b) ni kwa matumizi ya umma au ni kwa manufaa ya umma na inatekelezwa kwa mujibu wa Katiba hii au Sheria nyingine yoyote ya Bunge Kwamba–
    • (i) inahakikisha malipo kwa ukamilifu ya kumfidia mtu huyo kabla ya mali hiyo kuchukuliwa;
    • (ii) inampa mtu yeyote, mwenye maslahi au haki juu ya mali hiyo, njia ya kufikia mahakama ya kisheria.

(4) Sharti linaweza kuundwa ili kuruhusu fidia kulipwa kwa wakazi wa ardhi kwa nia nzuri chini ya ibara ya (3), ambao huenda hawana hatimiliki ya ardhi hiyo.

(5) Serikali itaunga mkono, kukuza na kulinda hakimiliki ya usomi kwa watu wa Kenya.

(6) Haki chini ya Kifungu hiki haijumlishi mali yoyote ambayo haijapatikana kisheria.