Ruka hadi Yaliyomo
AfroCave

Kifungu 34. Uhuru wa Vyombo vya Habari

(1) Uhuru na kujitegemea kwa vyombo vya matangazo, kuchapisha na vingine vya habari ya aina yoyote unahakikishwa lakini hauhusishi masharti yaliyotajwa katika Kifungu cha 33 (2) .

(2) Serikali–

  • (a) haitadhibiti au kuingilia mtu yeyote anayehusika na utangazaji, uchapishaji au usambazaji wa chapisho lolote au usambazaji wa habari kwa kutumia nyenzo yoyote; au
  • (b) haitamwadhibu mtu yeyote kwa kutoa maoni au mawazo au masuala yaliyomo kwenye matangazo, machapisho au usambazaji.

(3) Vyombo vya utangazaji na vyombo vingine vya habari na vya kielektroniki vina uhuru wa kujiendeleza kwa kuongozwa tu na taratibu za leseni ambazo–

  • (a) zimeratibiwa kuhakikisha udhibiti wa mawimbi ya hewa na aina nyingine za usambazaji wa mawimbi; na
  • (b) haviingiliwi na Serikali, maslahi ya kisiasa au ya kibiashara.

(4) Vyombo vyote vya habari vinavyomilikiwa na Serikali–

  • (a) vitakuwa huru kuamua kuhusu habari, tahariri na matangazo yao au mawasiliano mengine;
  • (b) havitaegemea upande wowote; na
  • (c) vitatoa nafasi sawa ya kuwasilisha maoni tofauti tofauti na mawazo yanayokinzana.

(5) Bunge litatunga sheria itakayotoa nafasi ya kuanzisha shirika ambalo–

  • (a) litakuwa huru dhidi ya udhibiti wa Serikali au kuingiliwa kisiasa;
  • (b) litaangazia maslahi ya sekta zote za jamii; na
  • (c) litaweka viwango na kudhibiti vyombo vya habari na kutathmini uzingativu wa viwango hivyo.