Ruka hadi Yaliyomo
AfroCave

Kifungu 15. Uraia kwa Kujiandikisha

(1) Mtu ambaye ameolewa na raia kwa muda wa angalau miaka saba ana haki, kutuma maombi ya kusajiliwa kama raia.

(2) Mtu ambaye amekuwa mkazi halali nchini Kenya kwa muda wa miaka saba mfululizo, na ambaye anatimiza masharti yote ya sheria yaliyoidhinishwa na Bunge, anaweza kutuma maombi ya kujiandikisha kama raia.

(3) Mtoto ambaye si raia na ambaye ni wa kupangwa na raia, ana haki ya kuwa raia kwa kutuma maombi.

(4) Bunge litatunga sheria itakayotoa masharti ambayo yatazingatiwa kuwapa uraia watu binafsi ambao ni raia wa nchi nyingine.

(5) Kifungu hiki kitatumika kwa mtu kuanzia tarehe ya kuanza kutumiwa kwa Katiba hii, lakini mahitaji yoyote ambayo ni lazima yatimizwe kabla ya mtu anayestahili kusajiliwa kama raia, yatachukuliwa kama yaliyotimizwa pasi na kuzingatia iwapo mtu huyu aliyatimiza kabla au baada ya tarehe ya kuanza kutekelezwa kwa Katiba hii, au kwa kiwango fulani kabla au baada ya tarehe ya kutekelezwa.