Ruka hadi Yaliyomo
AfroCave

Kifungu 237. Tume ya Kuwaajiri Walimu

(1) Tume ya Kuwaajiri Walimu imeundwa.

(2) Majukumu ya Tume ni–

  • (a) kusajili walimu waliohitimu;
  • (b) kuteua na kuajiri walimu waliosajiliwa;
  • (c) kuwapa kazi walimu walioajiriwa na Tume hii kuhudumu katika shule yoyote ya umma au taasisi;
  • (d) kuwapandisha vyeo na kuwahamisha walimu;
  • (e) kushughulikia masuala ya kinidhamu ya walimu; na
  • (f) kuwafuta kazi walimu.

(3) Tume–

  • (a) itachunguza viwango vya elimu na mafunzo kwa watu wanaojiunga na taaluma ya ualimu;
  • (b) itachunguza kuhitajika kwa walimu na upatikanaji wao; na
  • (c) itashauri serikali ya kitaifa kuhusu masuala yanayohusiana na taaluma ya ualimu.