Ruka hadi Yaliyomo
AfroCave

Kifungu 204. Hazina ya Usawazishaji

(1) Kutaundwa Hazina ya Usawazishaji ambayo itachukua asilimia moja unusu ya mapato yote yanayozalishwa na serikali ya kitaifa kila mwaka, katika misingi ya ukaguzi wa hesabu za mapato uliofanywa karibuni zaidi, kama itakavyoidhinishwa na Baraza la Kitaifa.

(2) Serikali ya kitaifa itatumia hazina ya kusawazisha kutoa huduma za kimsingi zikiwa ni pamoja na maji, barabara, matibabu na umeme katika maeneo yaliyotengwa hadi kiwango kitakachoboresha huduma hizo katika maeneo hayo kiwe sawa na kiwango kilicho maeneo mengine, iwezakanavyo.

(3) Serikali ya kitaifa inaweza kutumia Hazina ya Kusawazisha–

  • (a) iwapo matumizi ya fedha za hazina hiyo yameidhinishwa tu katika Mswada wa Matumizi ya Fedha uliopitishwa na Bunge; na
  • (b) ama kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja kupitia kwa misaada yenye masharti ambayo inahusisha makundi yaliyotengwa.

(4) Tume ya Ugavi wa Mapato itashauriwa na mapendekezo yake kutiliwa maanani mbele ya Bunge ili kupitisha mswada wa kuidhinisha matumizi ya fedha katika Hazina ya Usawazishaji.

(5) Fedha zozote ambazo hazitakuwa zimetumiwa katika Hazina ya Usawazishaji, zitasalia katika hazina hiyo kwa matumizi kwa mujibu wa ibara ya (2) na (3) katika mwaka wa fedha utakaofuata.

(6) Kifungu hiki kitaisha baada ya miaka ishirini kuanzia tarehe kitakapoanza kutekelezwa, kutegemea ibara ya (7).

(7) Bunge linaweza kupitisha sheria ya kuondoa utekelezaji wa ibara ya (6) kwa kipindi cha ziada cha miaka mahususi, kutegemea ibara ya (8).

(8) Kupitisha sheria katika ibara ya (7) lazima kuungwe mkono na zaidi ya nusu ya wabunge wote wa Baraza la Kitaifa, na zaidi yanusu ya wajumbe wa serikali za kaunti katika Seneti.

(9) Fedha hazitaondolewa katika Hazina ya Usawazishaji hadi pale Msimamizi wa Bajeti atakapoidhinisha kutolewa kwake.