Ruka hadi Yaliyomo
AfroCave

Kifungu 193. Sifa za Wagombea Uanachama wa Baraza la Kaunti

(1) Labda azuiwe na ibara ya (2), mtu atahitimu kugombea uanachama katika baraza la kaunti kama–

 • (a) amesajiliwa kama mpiga kura;
 • (b) anatimiza mahitaji yote ya kielimu, tabia nzuri na maadili mema kama inavyotakikana kwa mujibu wa Katiba au Sheria ya Bunge; na
 • (c) ama–
  • (i) ameteuliwa na chama cha kisiasa; au
  • (ii) ni mgombeaji wa kujitegemea aliyeungwa mkono na watu mia tano waliosajiliwa kama wapiga kura katika wadi husika.

(2) Mtu hataruhusiwa kugombea kiti katika baraza la kaunti iwapo mtu huyo–

 • (a) ana cheo Serikalini au afisi ya umma, mbali na hiyo ya baraza la kaunti anayowania kiti;
 • (b) amekuwa na cheo katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, wakati wowote ule katika miaka mitano iliyotangulia tarehe ya uchaguzi.
 • (c) hajakuwa raia wa Kenya kwa miaka isiyopungua kumi iliyotangulia tarehe ya uchaguzi;
 • (d) hana akili timamu;
 • (e) ni mufilisi;
 • (f) anatumikia kifungo gerezani cha miezi sita au zaidi; au
 • (g) amepatikana , kulingana na sheria yoyote, kwamba ametumia vibaya afisi ya umma ama kwa njia yoyote ile kukiuka kanuni za Sura ya sita.

(3) Mtu hatazuiwa kulingana na ibara ya (2) ila tu kama uwezekano wa kukata rufaa ama kesi yake kushughulikiwa upya kwa kifungo chake na mbinu zote za kujitetea zimekwisha.