Ruka hadi Yaliyomo
AfroCave

Kifungu 191. Mkinzano wa Sheria

(1) Kifungu hiki kinahusu mikinzano ya sheria kati ya sheria za kitaifa na zile za kaunti, kwa mujibu wa masuala yanayopatikana katika viwango vyote viwili vya Serikali.

(2) Sheria ya kitaifa itakuwa na mamlaka juu ya ile sheria ya kaunti iwapo–

  • (a) sheria za kitaifa zitatumika kwa usawa katika Kenya nzima na masharti mengine yaliyomo katika ibara ya (3) yametoshelezwa; au
  • (b) sheria za kitaifa zinalenga kudhibiti maamuzi yasiyo ya busara ya kaunti ambayo-
    • (i) yanaweza kuwa na athari mbaya kiuchumi, kiafya ama maslahi ya usalama wa Kenya au kaunti nyingine; au
    • (ii) zitazuia utekelezaji wa sera za uchumi wa kitaifa.

(3) Masharti yanayotajwa katika ibara ya (2) (a) ni yafuatayo–

  • (a) sheria za kitaifa hushughulikia suala ambalo haliwezi kutatuliwa na sheria zilizotungwa na kaunti peke yake.
  • (b) sheria za kitaifa hushughulikia suala ambalo ili lishughulikiwe kikamilifu, linataka sheria ambazo ni sawa katika taifa zima. Hufanya hivi kwa kuwa na-
    • (i) Kanuni na viwango vya ubora; au
    • (ii) sera za kitaifa; au
  • (c) Sheria za kitaifa ni muhimu kwa-
    • (i) uhifadhi wa usalama wa kitaifa;
    • (ii) uhifadhi wa umoja wa kiuchumi;
    • (iii) kulinda masoko ya pamoja kulingana na uhamishaji wa bidhaa, huduma na ufanyaji kazi, mtaji na ajira;
  • (iv) kuhimiza shughuli za kiuchumi miongoni mwa mipaka ya kaunti;
  • (v) kuhimiza nafasi sawa au usawa katika kufikia huduma za serikali; au
  • (vi) kulinda mazingira.

(4) Sheria za kaunti huwa na mamlaka juu ya sheria za taifa kama mahitaji yoyote yanayorejelewa katika ibara ya (2) hayahusiki.

(5) Katika kushughulikia mzozo unaohusu sheria za viwango tofauti zaserikali, mahakama yatapendelea ufasiri wa sheria ambao utazuia mzozo kuliko ufasiri ambao utaleta mzozo.

(6) Uamuzi wa mahakama kwamba sheria ya kiwango kimoja cha Serikali kinakubalika kuliko kifungu kingine cha sheria ya kiwango kingine cha Serikali hakubatilishi kifungu cha sheria cha kiwango kile kingine, ila tu sheria hiyo nyingine inakuwa haifanyi kazi kwa kiasi kile inachotofautiana na hiyo nyingine.