Ruka hadi Yaliyomo
AfroCave

Kifungu 177. Wanachama wa Baraza la Kaunti

(1) Baraza la kaunti lina wanachama wafuatao–

  • (a) wanachama waliochaguliwa na wapiga kura waliosajiliwa katika wadi, kila wadi ikijumuisha eneo moja la uwakilishi siku ile ya kupiga kura ya uchaguzi mkuu wa kuwachagua wabunge, itakayokuwa Jumanne ya pili ya mwezi Agosti baada ya kila miaka mitano.
  • (b) idadi ya wabunge maalum ili kuhakikisha kuwa hakuna zaidi ya wabunge thuluthi mbili wa jinsia moja katika bunge hilo.
  • (c) idadi ya wanachama kutoka katika makundi yaliyotengwa, wakiwemo watu walemavu, jamii za watu wachache na vijana, kama inavyopendekezwa katika Sheria ya Bunge; na
  • (d) spika, asiye mwanachama rasmi.

(2) Wanachama wanaotajwa katika ibara ya (1) (b) na (c) watatateuliwa na vyama vya kisiasa kwa mgao wa kutegemea idadi ya viti chama cha kisiasa kilivyopata katika uchaguzi huo, katika kaunti hiyo chini ya Ibara ya (a) kulingana na kifungu cha 90.

(3) Kujaza viti maalum kwa mujibu wa ibara ya (1) (b) kutaamuliwa baada ya kutangazwa kwa wanachama waliochaguliwa katika kila wadi.

(4) Baraza la kaunti huchaguliwa kwa kipindi cha miaka mitano.