Ruka hadi Yaliyomo
AfroCave

Kifungu 163. Mahakama ya Juu

(1) Kutabuniwa Mahakama ya Juu itakayojumuisha–

 • (a) Jaji Mkuu, ambaye atakuwa rais wa mahakama hiyo;
 • (b) Naibu Jaji Mkuu, ambaye –
  • (i) atakuwa naibu wa Jaji Mkuu; na
  • (ii) atakuwa Naibu wa rais wa mahakama hiyo; na
 • (c) majaji wengine watano.

(2) Mahakama ya Juu itakuwa imebuniwa kisawasawa kwa minajili ya kesi zake iwapo itakuwa na majaji watano.

(3) Mahakama ya Juu–

 • (a) itakuwa na mamlaka ya kipekee ya kusikiliza na kuamua kesi zinazohusu kura za afisi ya Rais zinazotokana na Kifungu cha 140; na
 • (b) kulingana na ibara ya (4) na (5), mamlaka ya rufaa ya kusikiza na kuamua rufani kutoka–
  • (i) Mahakama ya Rufaa; na
  • (ii) mahakama yoyote nyingine au mahakama maalum kama inavyoidhinishwa na sheria ya kitaifa.

(4) Rufaa zitakatwa kutoka kwa Mahakama ya Rufaa–

 • (a) Kwa misingi ya haki katika kesi yoyote inayohusisha ufasiri na utekelezaji wa Katiba hii; na
 • (b) katika kesi nyingine yoyote ambapo Mahakama ya Juu au Mahakama ya Rufaa inathibitisha kwamba suala muhimu kwa umma linahusika, kwa mujibu wa Ibara ya (5).

(5) Uamuzi wa Mahakama ya Rufaa chini ya ibara ya (4) (b) unaweza kuangaliwa upya na Mahakama ya Juu, kuukubali, kuurekebisha au kubadilishwa ama kubatilishwa.

(6) Mahakama ya Juu inaweza kutoa maoni ya ushauri kwa serikali ya taifa, taasisi yoyote ya serikali, au idara yeyote ya serikali ya kaunti iwapo itaombwa kufanya hivyo.

(7) Mahakama nyingine zote, isipokuwa Mahakama ya Juu, zitafuata maamuzi ya Mahakama ya Juu.

(8) Mahakama ya Juu itatunga sheria zitakazoongoza utekelezaji wa majukumu yake.

(9) Sheria ya Bunge inaweza kutoa masharti zaidi kuhusu majukumu ya Mahakama ya Juu.