Ruka hadi Yaliyomo
AfroCave

5. Tume ya Utekelezaji wa Katiba

(1) Tume ya Utekelezaji wa Katiba imeundwa.

(2) Tume inahusisha–

 • (a) Mwenyekiti; na
 • (b) Wanachama wengine wanane.

(3) Wanachama wa Tume–

 • (a) ni pamoja na watu wenye tajriba katika uongozi wa umma, haki za binadamu na serikali; na
 • (b) haitahusisha mtu yeyote aliyekuwa mwanachama katika Tume ya wataalamu iliyoteuliwa chini ya Sheria ya Marekebisho ya Katiba ya Kenya, 2008.

(4) Vifungu vya 248 hadi 254 vinahusu Tume hii.

(5) Baada ya Tume ya Ugavi wa Mapato kuundwa, Tume ya Utekelezaji wa Katiba itatuma taarifa za mikutano kwa Tume hiyo , na mwanachama wa Tume ya Ugavi wa Mapato ataruhusiwa kuhudhuria na kushiriki katika mikutano yoyote kama hiyo, lakini hatapiga kura.

(6) Majukumu ya Tume hii yatakuwa–

 • (a) kuchunguza, kusimamia na kuhimiza utungaji wa sheria na hatua zinazohitajika katika kutekeleza Katiba hii;
 • (b) kushirikiana na Mwanasheria Mkuu na Tume ya Marekebisho ya Sheria ya Kenya katika kutayarisha sheria itakayowasilishwa Bungeni ambayo itahitajika ili kutekeleza katiba hii; na
 • (c) kutoa ripoti za kila mara kwa Tume ya Kusimamia Utekelezaji wa Katiba kuhusu–
  • (i) hatua katika utekelezaji wa katika; na
  • (ii) vizuizi vyovyote katika utekelezaji wake; na
 • (d) kufanya kazi na kila Tume ya kikatiba kuhakikisha kuwa nia ya Katiba hii imeheshimiwa.

(7) Tume ya Utekelezaji wa Katiba hii itavunjwa miaka mitano tangu kuundwa kwake au baada ya kutekelezwa kikamilifu kwa Katiba hii kama itakavyoamuliwa na Bunge, yoyote ijayo mwanzo, lakini Baraza Kuu la Kitaifa, linaweza kufanya uamuzi wa kuiongezea muda.